Ingawa Carlos Tevez anatarajiwa kurudi Jijini Manchester Jumanne na kuanza mazoezi huku Meneja wa Manchester City Roberto Mancini akiungama Mchezaji huyo mpiganaji Uwanjani atawasaidia kwenye juhudi zao kujaribu kuupokonya Ubingwa toka kwa Mabingwa Manchester United, Tevez amekumbushia chimbuko la bifu lake na Mancini kwa kudai Mtaliana huyo alimtendea vibaya na kumwona mbwa wakati ugomvi wao uliolipuka kwenye mechi huko Ujerumani Mwezi Septemba ambako Man City walinyukwa 2-0 na Bayern Munich.
Tangu Siku hiyo Tevez hajachezea tena Man City, alipigwa Faini na yeye kuamua kurudi kwao Argentina bila ruhusa ya Klabu lakini hayo yanaelekea kumalizwa baada ya Mancini na upande wa Tevez kudokeza muafaka.
Hata hivyo, akiongea kwa uchungu kuhusu kiini cha mzozo huo, Tevez alibainisha chanzo ni Mancini kugombana na Straika Edin Dzeko ambae alitolewa na Kocha huyo ili kumwingiza Nigel de Jong huku Man City wakiwa washachapwa 2-0 na Bayern Munich.
Wakati huo Tevez anasema alishakuwa amepasha kwa Dakika 10 na pale Mancini alipoamrisha Dzeko atoke aingie De Jong yeye alirudi benchi kukaa na ndipo Dzeko alitoka huku akiwa amekasirika na kuaanza kupandishiana na Mancini na Mchezaji huyo kutoka Bosnia akaamua kwenda Vyumba vya Kubadilishia Jezi lakini ikabidi arudi benchi kwani huko Vyumbani milango ilikuwa imefungwa na akakaa jirani na Mancini.
Tevez akaeleza: ‘Dzeko alikuwa akiongea Kibosnia na Mancini akitukana Kitaliana! Ilikuwa vurugu! Akageuka na kuniona mimi! Akaamua kuniamrisha kama mbwa nipashe tena, nikamwambia siendi! Huwezi kunifanya mie mbwa! Nilikuwa tayari kucheza lakini Kocha alikuwa ameghadhibika na Dzeko na kuniparamia mie, kunitukana kusema maneno mabaya sana! Ukiangalia video utaona mie nimetulia tu na naongea na Pablo Zabaleta tu!’