Katika mechi ya marudiano ya Robo Fainali ya Copa del Rey iliyochezwa Uwanja wa Nou Camp jana usiku Barcelona walitoka sare na Real Madrid ya mabao 2-2 lakini Real wamebwagwa nje kwa vile Barcelona waliichapa Real bao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Wiki iliyopita.
Barcelona wamesonga kwenye Nusu Fainali kwa jumla ya mabo 4-3 na watakutana na mshindi kati ya Valencia au Levante ambao wanacheza leo usiku huku Valencia wakiwa mbele baada ya kushinda mechi ya kwanza mabao 4-1.
Katika mechi ya jana, hadi mapumziko Barcelona walikuwa mbele kwa bao 2-0 kwa bao za Pedro na Dani Alves lakini Real Madrid walizinduka kipindi cha pili na kusawazisha kwa bao za Cristiano Ronaldo na Karim Benzema.
Kwenye mechi hiyo Sergio Ramos wa Real alitolewa kwa Kadi Nyekundu kwa kumpiga kipepsi Kiungo wa Barca Sergio Busquets.
Katika mechi 14 walizocheza hivi mwishoni Real Madrid wameweza kuifunga Barca mara moja tu na hiyo ilikuwa hapo Aprili 20, Mwaka 2011 katika Fainali ya Copa del Rey waliposhinda bao 1-0 kwa bao la Cristiano Ronaldo.

![]() |