Kocha wa Rela Madrid Jose Mourinho amekubali kuwa wa kulaumiwa ni yeye kufuatia kipigo cha bao 2-1 walichoshushiwa na Barcelona jana usiku kwenye mechi ya kwanza ya Robo Fainali ya Copa del Rey iliyochezwa Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Kwenye mechi hiyo, Real walitangulia kupata bao mapema alilopachika Cristiano Ronaldo lakini kichwa cha Carles Puyol na bao la Eric Abidal ziiliwaua Real waliokuwa nyumbani kwao na mwishoni walitoka Uwanjani huku wakizomewa na Mashabiki wao wenye hasira.
Lakini Mourinho amepuuzi hatua ya Mashabiki hao na badala yake amekubali kulaumiwa kwa kutamka: ‘Naelewa nini kinaendelea kwa Mashabiki lakini huwa siwasikilizi kabla au baada ya mechi. Timu yangu ikifungwa mie ndio wa kulaumiwa! Ushindi siku zote una Baba wengi, lakini kipigo kina Baba mmoja tu. Nipo kwenye Soka muda mrefu na nalielewa hilo! Tulipotwaa Kombe hili wote tulishangilia, leo tumefungwa mimi ndio Mzazi pekee!’
Pia Mourinho amekiri kuwa Mchezaji wake Pepe huenda akaadhibiwa kwa kumtimba Lionel Messi mkononi wakati Messi alipokuwa yuko chini.
Wakati huo, Pepe alikuwa tayari ameshalambwa Kadi ya Njano kwa rafu mbaya kwa Sergio Busquets katika Kipindi cha Kwanza na angeweza kutolewa kwa Kadi Nyekundu zikiwa zimebaki Dakika 20 laiti kama Refa angeliona akimkanyaga Messi.

![]() |