Licha ya Klabu zote mbili, Manchester United na Liverpool, kudokeza kuwa Luis Suarez, ambae alifungiwa mechi 8 kwa ubaguzi wake dhidi ya Patrice Evra, atapeana mkono na Evra kabla ya mechi yao ya jana iliyochezwa Old Trafford na Liverpool kunyukwa bao 2-1 na Manchester United, Suarez alionyesha dhahiri dharau yake kwa Evra, Klabu yake na Wadau wote wa Soka pale alipoukataa mkono wa Evra wakati Timu hizo mbili zilipokuwa zikisalimiana kabla mechi kuanza.
Kitendo cha Suarez kilimfanya Evra aukamate mkono wa Straika huyo wa Liverpool lakini bado aligoma kumpa mkono Evra.
Tukio hili la kusikitisha liliwafanya Wahezaji wa Man United waliofuatia kina Rio Ferdinand, Valencia na Welbeck nao wagome kumpa mkono Suarez.
Kitendo hiki kimezua mjadala huku wengine wakimlaumu na kumponda Mchezaji huyo wa Liverpool.
Haya ni baadhi ya yaliyosemwa:
=Sir Alex Ferguson: ‘Huyu ni aibu na fedheha kwa Liverpool! Asiruhusiwe kuichezea Liverpool tena! Angezua ghasia!’
=Gordon Taylor, Mkuu wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa: ‘Ni kukosa heshima, haikufaa na inaaibisha!’
=Rio Ferdinand: ‘Nimepoteza heshima yote kwake! Hastahili heshima huyu, yangekwisha haya kwa kupeana mkono!’
=Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Alan Hansen: ‘Kabla ya mechi tuliambiwa na Liverpool atapeana mkono na Evra, sasa kwa kukataa hilo ni kitendo kisichokubalika!’
=John Barnes, Mchezaji wa zamani wa Liverpool: ‘Nilpoona laivu amekataa kutoa mkono, nilishangazwa!’
=Kenny Dalglish, Meneja wa Liverpool, baada ya mechi, alidai: ‘Nilikuwa sijui kama Suarez alikataa kumpa mkono Evra! Sikuwepo, na sikuona! Ni kinyume na nilichoambiwa!’
Hata hivyo, licha ya dharau hii ya Suarez, habari toka FA zinabaini hamna hatua yeyote ambayo Suarez anaweza kuchukuliwa kwa vile kupeana mikono ni hiari na hili nalo limeanzisha mdahalo mwingine wa kwamba ikiwa hivyo ndivyo sasa kwa nini Timu zisalimiane kabla ya mechi.