Fabio Capello amejiuzulu kama Meneja wa Timu ya Taifa ya England kama ilivyothibitishwa na Chama cha Soka England, FA.
Kujiuzulu kwa Capello kunafuatia mkutano wake wa leo na Mwenyekiti wa FA David Bernstein na Katibu Mkuu Alex Horne kikao ambacho kimekuja baada ya Capello kumpinga Mwajiri wake, FA, kwa kumng’oa Unahodha wa England Mchezaji wa Chelsea John Terry ambae anasubiri kuburuzwa Mahakamani hapo Julai 9 kukabili mashitaka ya kumtukana kibaguzi Beki wa QPR Antoin Ferdinand, ambae ni mdogo wa Rio Ferdinand wa Manchester United, wakati QPR ilipoifunga Chelsea bao 1-0 katika mechi ya Ligi iliyochezwa Oktoba Mwaka jana.
Mara baada ya kuamuliwa Terry ana Kesi ya kujibu Mahakamani kulizuka mjadala mkubwa huko England uliotaka aondolewe kama Nahodha wa Timu ya Taifa huku wengine wakitaka asichezee kabisa England hadi Kesi yake imalizike.
England itacheza michuano mikubwa ya EURO 2012 Mwezi Juni kugombea Ubingwa wa Ulaya itakayofanyika huko Poland na Ukraine wakati Kesi ya Terry itaanza Julai 9 ikiwa ni Siku 9 baada ya EURO 2012 kumalizika..
FA imesema itatoa taarifa kamili kuhusu kung’oka kwa Capello katika mkutano na Wanahabari utakaofanyika Uwanja wa Wembley, London Alhamisi Saa 8 mchana, bongo taimu.