Rooney: ‘EUROPA haipoteze lengo letu kutwaa Ubingwa!’
Wayne Rooney ameweka msisitizo kuwa kushiriki kwao EUROPA LIGI hakutaua azma yao ya kutaka kuutwaa Ubingwa wa England kwa mara ya 20 Msimu huu.
Ikiwa Manchester United watafika Fainali ya EUROPA LIGI itabidi wacheze mechi 8 za Mashindano hayo ya Ulaya pamoja na Mechi 13 walizobakisha kwenye Ligi Kuu England ili kutetea Ubingwa wao.
Lakini Rooney amesema: ‘Haituzuii kutwaa Ubingwa England, tumezoea mechi kubwa na nyingi. Hamna haja ya kushiriki michuano ikiwa hutaki kushinda! Itakuwa mara ya kwanza Man United kutwaa EUROPA na tunalitaka Taji hili!’
Wenger: ‘Arsenal tushikamane!’
Bosi wa Arsenal Arsene Wenger ametaka Klabu yake wabaki wamoja na kupigana kufuatia kutupwa nje ya FA Cup hapo Jumamosi waliponyukwa 2-0 na Sunderland kipigo ambacho kilikuja Siku 3 tu baada ya kuchapwa 4-0 huko San Siro na AC Milan kwenye UEFA CHAMPIONZ LIGI na kuwaacha kwenye hati hati kubwa ya kumaliza Msimu huu bila Taji lolote, hasa kwa vile kwenye Ligi nako wako nafasi ya 4 Pointi 17 nyuma ya vinara, na ikiwa watakosa Taji huu utakuwa ni Mwaka wa 7 mfululizo bila Kombe lolote.
Wenger ametamka: ‘Tumekubali kulaumiwa, kilichobaki tushikamane na kuwakabili hao wanaotulaumu. Ni ngumu kusema hili limetuweka wapi lakini tutapigana!’
Aliongeza: ‘Lazima tutilie mkazo gemu inayokuja, tumalize Ligi juu na tufanye vizuri kwenye UEFA CHAMPIONZ LIGI ingawa nafasi finyu.’
Mechi ijayo ya Arsenal ni Jumapili ijayo watakapokuwa Emirates kucheza na Mahasimu wao wa London ya Kaskazini Tottenham kwenye Ligi.
Drogba: ‘Huu ni Msimu mgumu kupita yote!’
Straika wa Chelsea Didier Drogba ameungama kuwa Msimu huu ndio mgumu kupita Misimu yote tangu awepo hapo Stamford Bridge.
Chelsea wamekuwa na matokeo ya kusuasua Msimu huu ingawa bado wamo kwenye vinyang’anyiro vya FA Cup na UEFA CHAMPIONZ LIGI huku Meneja wao Kijana Andre Villas-Boas akianza kupata joto ya jiwe.
Jana Chelsea nusura watupwe nje ya FA Cup kama si Daniel Sturridge kusawazisha na kutoka 1-1 na Birmigham City kwenye Raundi ya 5 na kulazimisha marudiano ambayo yatachezwa huko Uwanja wa Mtakatifu Andrew hapo Machi 6.
Drogba, ambae alijiunga na Chelsea Mwaka 2004 akitokea Marseille ya Ufaransa, amesema: ‘Huu ni Msimu mgumu tangu nije hapa. Wachezaji na Mashabiki wamezoea kuwa nafasi za juu za kwanza au za pili au za tatu lakini sasa ni tofauti!’