Wakati kuna taarifa mbaya kwa Arsenal kufuatia Sentahafu wao wa Kimataifa kutoka Ujerumani, Per Mertesacker, kufanyiwa opersheni ya enka itakayomweka nje pengine kwa Msimu wote uliobaki, Kiungo wa zamani wa Klabu hiyo, Emmanuel Petit, amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya baadae ya Arsenal na inabidi kuwaondoa baadhi ya Wachezaji na kuwaleta Wachezaji 6 wazuri wanaosifika.
Akithibitisha habari za Mertesacker, Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema Beki huyo amepasuliwa enka na atakuwa nje kwa muda mrefu.
Mertesacker aliumia Jumamosi iliyopita huko Stadium of Light kwenye mechi ya Ligi Arsenal walipoifunga Sunderland 2-1.
Pamoja na Mertesacker, Sentahafu mwenzake Laurent Koscielny atakuwa nje kwa Wiki moja.
Nae Emmanuel Petit, ambae alikuwa hapo Arsenal kati ya Mwaka 1997 na 2000 akishirikiana kwenye Kiungo na Patrice Vieira, amedai Wachezaji kama Andrei Arshavin, Tomas Rosicky na Theo Walcott sio wazuri na inabidi wafunguliwe mlangp waondoke.
Akikiri kuondoka kwa Cesc Fabregas na Samir Nasri kumewaathiri Arsenal, Petit alisema: ‘Timu iko hali mbaya kupita nilivyodhani.’
Juzi Jumatano huko San Siro, Milan, Arsenal, ikicheza mechi ya kwanza ya Raundi ya Mtoano ya UEFA CHAMPIONZ LIGI, ilichapwa bao 4-0 na AC Milan na Jumamosi wapo ugenini kucheza na Sunderland kwenye Raundi ya 5 ya FA Cup.