Leo Saa 10 jioni, Yanga , Mabingwa wa Soka Tanzania Bara, wanatinga Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kuivaa Zamalek ya Misri, ambao ni Mabingwa wa zamani wa Afrika waliotwaa Taji hilo mara 5, katika mechi ya Raundi ya Awali ya CAF Championz Ligi na pambano hili limeufanya Mji wote wa Dar es Salaam ujae hisia kali kwa Washabiki wa Soka huku wengine wakiwa na sikio lao huko Kigali, Rwanda ambako wakongwe wengine wa Soka Simba watakuwa wakicheza mechi yao ya kwanza ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Kiyovu ya huko.
Katika mahojiano na Wanahabari hapo jana, Kocha Msaidizi wa Zamalek, Ossama Nabil alisema wao wapo hapa si kutafuta ushindi tu bali lengo lao ni kutwaa Ubingwa wa Afrika ambao waliuchukua mara ya mwisho Mwaka 2002.
Nae Kocha wa Yanga, Kostadin Papic, ametamka: ‘Kama kocha nimemaliza kazi yangu, ninaweza kusema tupo tayari kupambana na Zamalek katika pambano hili gumu. Hatuna la zaidi uwanjani zaidi ya ushindi!’
Mbali ya wakongwe hawa Yanga na Simba, Timu za Zanzibar, Mafunzo na Jamhuri, nazo zitaingia uwanjani kwa Mafunzo kucheza na Liga Muculmana de Maputo ya Msumbiji katika CAF CHAMPIONZ LGI na Jamhuri kuivaa Hangwe ya Zimbabwe kwenye Kombe la Shirikisho.
MUNGU IBARIKI TANZANIA!