Waziri Mkuu wa Misri, Kamal el-Ganzouri, ameitimua Bodi ya Shirikisho la Soka la Misri, EFF, na kuagiza Memba wake wahojiwe na Polisi kufuatia maafa ya vurugu zilizosababisha zaidi ya Watu 70 kufa hapo jana huko Mjini Port Said mara baada ya mechi ya Ligi kati ya Al-Masry na Al-Ahly.
Sambamba na uamuzi huo pia Gavana wa Port Said na Mkuu wake wa Polisi wamejiuzulu huku Ligi zote huko Misri zikisimamishwa kwa muda usiojulikana.
Inadaiwa mara baada ya mechi hiyo kumalizika huku Al-Masry ikiifunga Al-Ahly bao 3-1 washabiki waliokuwa na fimbo na visu walivamia uwanja huku Polisi wa kutuliza ghasia wakiwaangalia tu.
Wakati FIFA imetaka uchunguzi kamili ufanyike, Rais wake Sepp Blatter amesema hiyo ilikuwa siku mbaya mno kwa soka.
Nae Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika, CAF, Issa Hayatou, akiagiza kuwa kabla ya mechi za Robo Fainali za AFCON 2012 zitakazochezwa Jumamosi na Jumapili huko Gabon na Equatorial Guinea kutakuwa na kusimama kimya kwa dakika moja ili kuomboleza na kutoa heshima kwa waliokufa, alisema: ‘Soka la Afrika liko kwenye maombolezo!’
Nae Kocha wa Al-Ahly, Manuel Jose kutoka Ureno, ambae amerudi kwao baada ya kupata mstuko mkubwa, alisikitika: ‘Nilipigwa ngumi na mateke shingoni, kichwani na miguuni. Kwenye Vyumba vya Kubadili Jezi niliona Mashabiki wetu wakifa na hatukuweza kusaidia lolote. Hakuna Mchezaji aliedhuriwa lakini tuna majonzi makubwa. Lazima nitazame upya maisha yangu hapa. Hili limebadilisha maisha yangu!’