Watu wasiopungua 74 wamefariki baada ya kutokea ghasia kwenye mechi huko Mjini Port Said, Misri kati ya Klabu ya mjini hapo Al-Masry na Vigogo wa Misri Al-Ahly ya Cairo.
Vurugu hizo zilitokea mara baada ya pambano kumalizika huku Al-Ahly ikiwa imechapwa bao 3-1 na Mashabiki kuvamia Uwanja kuwakimbiza Wachezaji na ndipo yakaanza mapambano ya Mashabiki wa pande hizo mbili.
Mbali ya vifo hivyo pia inasemekana Watu zaidi ya 100 wamejeruhiwa.
Akiongea baada ya vurugu hizo, Mchezaji mkongwe na anaheshimika huko Misri wa Al-Ahly na Timu ya Taifa, Mohamed Aboutrika, alisikitika: ‘Huu si mpira. Hii ni vita na Watu wanakufa mbele yetu. Naomba Ligi isimame. Hii ni hali mbaya sana na Siku hii haitasahaulika!’
Mara baada ya maafa hayo ya huko Port Said, Mjini Cairo pambano kati ya Zamalek na Al-Ismailiya lilivunjwa huku mechi ikiwa bao 2-2 ili kuomboleza maafa hayo.
Hata hivyo Washabiki wa Zamalek wenye hasira walianza vurugu kwa kuvunjika pambano hilo.
Baadae taarifa kutoka Kituo cha TV cha Serikali kilisema mechi za Ligi Kuu zitasimamishwa hadi baadae na Bunge litafanya Kikao maalum kujadili maafa hay.o
Yanga ya Dar es Salaam inatarajiwa kwenda huko Cairo mwanzoni mwa Mwezi Machi kurudiana na Zamalek ya Misri kwenye mechi ya CAF CHAMPIONZ LIGI baada ya kucheza mechi ya kwanza hapo Februari 18 Mjini Dar es Salaam.