Wakiwa njiani kwenda kupambana na Senegal kwenye mechi ya mchujo ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia, Kikosi kizima cha Timu ya Taifa ya Zambia kiliangamia katika ajali ya Ndege iliyotokea tarehe 27 Aprili 1993 Nchini Gabon mara baada ya kuruka toka Uwanja wa Ndege wa Libreville walikotua kujaza mafuta ili kuelekea Senegal.
Jumamosi Januari 21, Zambia watakuwa Mjini Bata, Equatorial Guinea kucheza na Senegal katika mechi yao ya ufunguzi ya Kundi A la Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mahala ambako si mbali sana na sehemu iliyotokea ajali ya Ndege iliyoteketeza Timu yao ya Taifa ambayo mpaka leo inadaiwa ndio ilikuwa bora kupita zote.
Kikosi cha sasa cha Zambia kimeahidi kucheza mechi hii na Senegal kwa ari kubwa ili kuwaenzi wenzao.
Kikosi hicho cha Zambia kilichoteketea kilianza kuwika kwenye michezo ya Olimpiki Mwaka 1988 wakati Kalusha Bwalya alipopiga hetitriki walipowachapa Italy 4-0
Kalusha Bwalya, akiwa kwao na Klabu ya Mufulira ‘aligunduliwa’ na Mbelgiji mmoja ambae alimpeleka kuchezea Brugge Cercle na, baada ya kuwika kwenye Olimpiki, PSV Eindhoven ikamsajili.
Uhamisho huo ndio uliokoa maisha ya Kalusha Bwalya.
Yeye na Charles Musonda, aliekuwa akichezea Anderlecht, iliamuliwa wasiende Zambia bali wasafiri moja kwa moja kutoka kwenye Klabu zao za Ulaya na kwenda Senegal ambako wangejiunga na wenzao.

![]() |