Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, leo limetoa taarifa kwamba Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilikutana Februari 15 Mwaka huu Jijini Dar es Salaam na kufanya uamuzi kwa ajenda mbalimbali ikiwemo Marekebisho ya Katiba za Wanachama wa TFF na pia ushauri wa kisheria ulioombwa kwake na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Kikao hicho kiliamua kwamba Wanachama wake wote 40 wa TFF wanatakiwa kufanya marekebisho kwenye Katiba zao katika maeneo matatu kwa mujibu wa maelekezo ambayo TFF ilitoa Mwaka jana.
Maeneo ambayo yanatakiwa kurekebishwa ni sifa za Wagombea uongozi ambapo kwenye kipengele cha elimu ni lazima iwe kuanzia Kidato cha Nne, kutopeleka masuala ya Soka Mahakama za kawaida na Kamati zao za Uchaguzi kutakiwa kufanya kazi chini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Kwa kuzingatia hayo TFF imeamua kuwa hakuna mwanachama yeyote wa TFF anaeruhusiwa kufanya Uchaguzi kwa sasa kama Katiba yake ina upungufu au inakwenda kinyume na maelekezo kuhusu maeneo hayo matatu.
Kamati hiyo imetoa hadi Juni Mosi Mwaka huu kwa Wanachama ambao Katiba zao zina upungufu katika maeneo hayo wawe wamefanya marekebisho ndiyo waendelee na Uchaguzi kwa wale ambao muda wa uchaguzi umefika.
Pia, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji imeishauri Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwamba Katiba zote za Wanachama ziwe na vitu hivyo vitatu vilivyotakiwa kufanyiwa marekebisho.
SIKU YA WANAWAKE DUNIANI- MACHI 8
Wakati huohuo TFF imetangaza kuwa Machi 8 kila mwaka ni Siku ya Wanawake Dunia na ili kuadhimisha siku hiyo kwa upande wa Soka, TFF kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) imeandaa Mashindano mafupi kwa Shule nane za Sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam.
Mashindano yataanza Februari 24 Mwaka huu kwenye Viwanja viwili vya Jitegemee Sekondari ambapo kutakuwa na Kundi B wakati kundi A litacheza mechi zake Makongo Sekondari.
Mechi zitaanza saa 8 mchana na kumalizika saa 10 jioni.
Kundi A lina shule za Makongo, Goba, Twiga na Lord Barden wakati Jitegemee, Benjamin Mkapa, Kibasila na Tiravi zitakuwa kundi B.
Kwa mujibu wa TFF, lengo la Mashindano hayo ni kuhamasisha Soka kwa Wasichana katika ngazi ya Shule, kuandaa, kubaini na kuendeleza mafanikio yanayopatikana katika Timu ya Wanawake ya Taifa.