TAARIFA HII IMESAHIHISHWA kutokana na mkanganyo wa RATIBA==Ni Mwezi mmoja tu umepita tangu ‘Timu Tajiri’ Azam FC ilipoichapa Simba bao 2-0 huko Zanzibar kwenye Mapinduzi Cup na Jumamosi watatinga tena Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kucheza mechi ya Ligi Kuu Vodacom ambayo inasubiriwa kwa hamu hasa kwa vile ushindi kwa Azam utaiengua Simba toka kileleni mwa Ligi ikiwa Yanga watashindwa kuifunga Mtibwa Sugar zaidi ya bao mbili watakapocheza hapo kesho.
Simba, iliyocheza mechi 16 kama Azam, ipo kileleni ikiwa na pointi 34 na Azam wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 32 huku Yanga wakishika nafasi ya 3 wakiwa na pointi 31 kwa mechi 15.
Huku wakitoka kwenye machungu ya hivi juzi kutunguliwa bao 1-0 na Timu inayosuasua kwenye Ligi Villa Squad iliyomaliza mechi hiyo Mtu 9 baada ya Wachezaji wake wawili kupewa Kadi Nyekundu, Simba, bila shaka, watajizatiti kwenye mechi hii.
Lakini Kocha wa Azam, Stewart Hall, anaetoka Uingereza, amesema anaijua Simba na nini udhaifu wake na kuahidi atatumia mbinu alizotumia Zanzibar kuifunga Simba.
Hall alinukuliwa akisema: ‘Siwahofii Simba, nina hakika nitaifunga tena. Nimeshafahamu udhaifu wa Timu hiyo, hakuna cha kunishinda kwao. Lakini ieleweke kuifunga Simba kila wakati haina maana ni Timu mbovu. Real Madrid kufungwa na Barcelona kila mara haimaanishi ni wabaya, kwenye soka mambo haya hutokea!’.