Katika hali inayoleta matumaini makubwa kwa Soka la Tanzania, Yanga imetangaza kujenga Uwanja wa kisasa utakaopakia Watazamaji 15,000 wote wakiwa vitini na pia jengo lenye ghorofa 7 miradi ambayo itawagharimu Shilingi Bilioni 10.
Uwanja huo wa kisasa utajengwa ulipo Uwanja wao wa sasa, Kaunda, maeneo ya Jangwani Jijini Dar es Salaam na jengo litajengwa Mtaa wa Mafia yalipokuwa Makao Makuu yao zamani na litakuwa na Maduka 20, Ofisi 20, Hosteli ya Vyumba 20 pamoja na Kliniki.
Taarifa za miradi hiyo zimetangazwa na Mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga, wakati wa kusaini Makubaliano ya Awali na NEDCO, National Estates and Designing.
Hata hivyo, Nchunga amesisitiza kilichosainiwa si Mkataba ambao utasainiwa pale tu pesa za Miradi hiyo zitakapopatikana.
Yanga inatarajia kupata hizo Shilingi Bilioni 10 kupitia michango na mikopo toka kwa Kampuni za nje na ndani.
Kwa sasa ni Azam FC tu yenye Uwanja wake huko Chamazi kwenye viunga vya Jiji la Dar es Salaam lakini katika Siku za nyuma Klabu ya Simba iliwahi kutangaza mipango ya kujenga Uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua Watazamaji 30,000 huko Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kusema ujenzi huo utasimamiwa na Kampuni ya Ujenzi ya Kituruki, GIDAS, ambao ni Mabingwa wa ujenzi wa Viwanja vya michezo.
Taarifa hizo za ujenzi huo zilitangazwa na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, ambae alisema Uwanja huo utazungukwa na Maduka ya kisasa ya mtindo wa ‘Mol’ [Mall].

Maoni