Tanzania Breweries Limited, TBL, kupitia Bia yake maarufu Kilimanjaro
Premium Lager, imetoa Vifaa vya michezo kwa Klabu kongwe Nchini, Yanga na Simba, ikiwa ni sehemu ya Udhamini wao wa Miaka mitano kwa Klabu hizo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 5.
Akizungumza kwenye makabidhiano hayo yaliyofanyika jana Makao Makuu ya TFF, George Kavishe, ambae ni Meneja wa Bia aina ya Kilimanjaro Premium Lager, alisema wao wana furaha kubwa kushirikiana na Klabu kubwa Nchini ili kuleta maendeleo ya michezo.
Klabu hizo mbili zilikabidhiwa Jezi, Viatu, Suti za Michezo, Glovu za Makipa, saa maalum za michezo pamoja na vifaa vingi vingine.
Wakitoa shukrani zao, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, aliisifu TBL kwa kutimiza Mkataba wao huku Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa, akisema hiyo ni changamoto kwao ili wapate mafanikio na pia kutetea Ubingwa wao.
